Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Muhammad Al-Farah, mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen, ametoa ujumbe kwa wanamgambo na mamluki wanaoiunga mkono Saudi Arabia, akiwataka wasikate njia zao za mawasiliano na Sana’a.
Alionya kwamba: Hesabu za Saudi zinaweza kubadilika pale ambapo maslahi na miundombinu muhimu ya ufalme huo vitatishiwa moja kwa moja.
Al-Farah aliandika katika mfululizo wa machapisho kwenye ukurasa wake binafsi katika jukwaa la «X» kwamba: Wanamgambo na mamluki wanaoiunga mkono Saudi Arabia wanapaswa kuzingatia katika hesabu zao uwezekano wa kukoma kwa mapambano kupitia makubaliano ya suluhu yatakayoilazimisha Riyadh kuachana na chaguo zake.
Aliwataka waache milango ya kurejea ikiwa wazi kwa ajili yao na wasitegemee kikamilifu uhamasishaji wa vikosi na maamuzi yanayotolewa kutoka nje.
Mwanachama huyo mwandamizi wa Ansarullah alitahadharisha dhidi ya kufuata kauli za vyombo vya habari zenye kuchochea, akibainisha kwamba: Baadhi ya watu wenye ushawishi wanaoishi nje ya Yemen na wanaofanya shughuli zao kutoka miji mikuu ya kikanda na kimataifa, wanawachochea wapiganaji kuongeza mvutano, wakati wao wenyewe wako mbali na medani za vita na madhara yake ya moja kwa moja.
Mwanachama huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alisisitiza: Saudi Arabia, pale gharama ya mapambano itakapoongezeka, itaweka maslahi yake, miundombinu yake, viwanja vyake vya ndege na usalama wake wa ndani katika kipaumbele cha hesabu zake, na haitakuwa tayari kubeba hasara kubwa kwa ajili ya kuwatetea mamluki na wanamgambo wa ndani wanaoihusisha nayo.
Mwanachama huyo wa Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah alihusisha kuendelea kwa msimamo wa Saudi Arabia wa kukataa matakwa ya Wayemen na msisitizo wa Riyadh wa kuendelea na ushawishi wake ndani ya Yemen na kudumisha mzingiro pamoja na shinikizo za kiuchumi na kisiasa.
Alifafanua: Kupuuza matakwa ya Yemen, licha ya kuongezeka kwa gharama za vita, kunaonyesha kushikilia chaguo ambazo, mbali na upande wa kijeshi, zinahusiana na jitihada za kudhibiti maamuzi ya Yemen.
Al-Farah, akiuliza kwa nini Saudi Arabia inakataa matakwa ya Yemen na haki zao halali, licha ya kujua kwamba kuendelea kuyakataa kunapandisha gharama ya mapambano na kuongeza hatari zinazoukabili ufalme huo na maslahi yake, alisema: Tafsiri ya suala hili ni kwamba Riyadh bado inataka kudumisha ushawishi wake nchini Yemen na kuhifadhi hali ya mzingiro na shinikizo; sambamba na hilo, Saudi Arabia iko chini ya shinikizo kutoka Marekani na nchi za Magharibi linalohusiana na masuala ya kikanda na misimamo yake kuhusu mzozo na utawala wa Kizayuni.
Aliongeza: Washington na utawala wa Kizayuni wanajaribu kuirejesha Yemen katika mikono ya Marekani na kuiweka ndani ya mfumo wa kikanda unaoendana na maslahi ya Marekani na Wazayuni.
Al-Farah aliongeza: Mwelekeo huu unalenga nguvu zinazochukua misimamo inayopinga utawala wa Marekani na kuunga mkono suala la Palestina. Shinikizo za nje zimesababisha maamuzi ya Saudi Arabia kuathiriwa na hesabu zinazozidi maslahi ya moja kwa moja ya nchi hiyo, kwa kuwa Riyadh inajiona ikikabiliwa na maagizo ya Marekani ambayo haiwezi kuyakataa kwa urahisi.
Maoni yako